Saturday, March 28, 2015

BINTI CHINI YA MIAKA 18, BADO NI MTOTO.


Miaka inaenda sana, na kwa sasa tupo katikati mwa karne ya 21, karne ambayo inaongozwa na mapinduzi ya taarifa au habari, kwa lugha ya kingereza inajulikana kama information age. Sasa hivi kufuatia kukua kwa teknolojia ya mawasilano, taarifa na habari nyingi husambaa kwa kasi zaidi, na kwa muda mfupi kuliko vile ilivyokua mwanzo, kwa maana hiyo maisha sasa yamebadirika sana, hivyo sisi Watanzania tunapaswa kukubali na kuendana na hali halisi ya maisha iliyopo kwa sasa. Hatuna budi kuachana na mila kandamizi zenye kuleta maumivu kwa wanawake na watoto ili tuweze kupambana kwenye karne hii ya 21 ya utandawazi kwa ujumla, kwasababu sasa dunia ni kama kijiji.Fursa zimeongezeka sana, lakini pia maovu mengi ni rahisi kuonekana Dunia nzima kwa muda mfupi sana, kuliko ilivyokua zamani.

Hakuna Taifa lililoendelea Duniani, ambalo Wanawake wake hawana Elimu,au hawajaenda shule. Hakuna taifa lililoendelea Duniani ambalo wanawake
wake waliozeshwa mapema na kukosa fursa ya kusoma, kufanya kazi na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yao, kuwaozesha mabinti mapema ni kukuza ukandamizaji wa wanawake na kuongeza Idadi ya Wanawake walio tegemezi nchini.

Ifike wakati, mtoto apate haki zake stahiki pasipo kuidai au kushurtisha wazazi na serikali watambue mahitaji yao kama inavyoonekana hapo kwenye picha, hao ni wasichana wa shule za sekondari huko shinyanga wakilia sana na kupinga wao kuolewa mapema huku wakisema "Hatutaki kuolewa, Tunataka kusoma". Kwa dunia hii ya sasa, yenye mapinduzi makubwa ya taarifa na habari, unapomnyima msichana fursa ya kusoma kwa kumuozesha mapema unamfanya awe tegemezi kwa wazazi au mwanaume atakae enda kuishi nae, ukijumuisha hali ngumu ya maisha iliyopo kwa sasa, kila kitu kina gharama kubwa, anapomtegemea mwanaume kwa kila kitu inaongeza unyanyasaji na matukio ya kikatili wanaofanyiwa wanawake kutokana hawawezi kuendesha maisha yao bila kuwategemea wanaume wao.
Watoto wote duniani huzaliwa sawa, na hufuata hatua zote za ukuaji kulingana na umri walionao na makuzi au mazingira waliyolelewa, hivyo kumuozesha au kushiriki kimapenzi na binti aliye na umri chini ya miaka 18, ni kumdhalisha na kumfanyia ukatili wa kingono, kwasababu maumbo yao ndiyo yamekua lakini upeo wao wa kufikiria na kuchanganua bado haujakua kiasi cha kufanya maamuzo sahihi kuhusiana na afya za miili yao. Hivyo jmii, wazazi na serikali tunajukumu la kuwalinda mabinti chini ya miaka 18, kuwaelimisha kuhusu afya zao na mahusiano ya kimapenzi chini ya umri wa miaka 18, na changamoto zake.



Friday, March 27, 2015

KURA YANGU NI CHACHU YA MAENDELEO!!!

Hii picha nilipiga mwezi wa 12 mwaka jana, mara baada ya kutekeleza Haki na wajibu

Wangu, mimi mtanzania kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi wa 12 mwaka jana. Watanzania wengi tumekua na tabia ya kulaumu tu kuwa viongozi waliopo madarakani hawatimizi wanayopaswa kuyafanya kama viongozi na wawakilishi wetu, lakini ukija kuangalia kwa kiasi kikubwa Watanzania tulio wengi hatushiriki katika kuwachagua viongozi ambao tunawalalamikia, huwenda kwa kutokujua au tu kupuuzia na matokeo yake  masuala mbalimbali ya kimaendeleo yamekua yakichelewa wakati mwengine kutokufanyika kabisa, na wakati mwengine madhara makubwa kutokea kwenye jamii yetu kutokana ba viongozi na watendaji wazembe waliopo.

Kura yangu inanafasi kubwa sana ya kubadilisha mambo mbalimbali yanayoizinguka jamii yangu, iwapo tutajijengea utamaduni wa kupiga kura, kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyo sasa basi matatizo mengi yaliyopo katika jamii kwa sasa yatatatulika kwasababu njia pekee ya kumuwajibisha mtu asiyetenda au kutimiza wajibu wake kiurahisi ni kwa kupitia sanduku la kura.
Sanduku hili litakuwa muamuzi wa kiutendaji wa watu tunaowapa dhamana ya kuwa wawakilishi wetu sehemu mbalimbali, na kwa namna hiyo viongozi wengi wataanza kuwajibika kwasababu sanduku la kura litakuwa linahusika kila baada ya awamu kuisha, kupima masuala yao ya kiutendaji, ikiwa ni pamoja na kwenda kinyume na vitu walivyoahidi au ambavyo walishindwa kutekeleza kabisa.
Wakati umefika sasa kwa wanawake kujua thamani ya kura zetu badala ya kuwapigia watu kura kwasababu ya kitu cha siku moja ambacho kitakuacha muda mrefu kuumia kutokana na utendaji wao mbovu, chagua mtu si kwasababu anakupa kitu, chagua mtu kwasababu anauwezo na vigezo vya kutimiza malengo ya sehemu ulipo, nchi uliyopo na mwenye uwezo wa kutatua changamoto tulizonazo.
Kuelekea uchaguzi mkuu, ifanye kura yako/yangu iwe chachu ya maendeleo yetu.


Wednesday, March 25, 2015

KAZI YEYOTE HALALI INAFAIDA

 Kumekua na wimbi kubwa sana la vijana wasiokuwana ajira, wengi wakiilalamikia serikali kutokana na tatizo hili la ajira, lakini wasichokijua ni kwamba kazi yeyote ya halali inafaida, si lazima mpaka uwe umeajiriwa serikalini au sekta binafsi ndiyo uweze kuendesha maisha yako, hata biashara na ujasiriamali unaweza kukufanya kuendesha maisha yako vizuri kuliko vile ambavyo ungeajiriwa na mtu.
Ukigusa tu suala la kujiajiri, wapo watakaokwambia unaanzaje kujiajiri wakati mtaji ni changamoto, napenda nitumie fursa hii kukwambia anza na ulicho nacho katika kutekeleza mipango yako mbalimbali ya kimaendeleo, usisubiri kuwezeshwa, anza wale wa kukuwezesha wawe wa ziada lakini si tegemezi kwako. Kwa mfano wewe huna mtaji ila unauwezo wa kusuka watu nywele, anza kwa kuwasuka watu nywele upate mtaji wa kuanzisha biashara yako, au unanguvu huna kazi au mtaji wa kufanya miradi yako uliyoipanga, anza kwa kutumia hizo nguvu zako kutafuta pesa itakayokuwezesha kupata mtaji, kama ni kumsaidia mtu kupika mama ntilie, kufyatua matofali, kuuza dagaa sokoni kama huyo mdada pichani we anza tu ili mradi ujue kabisa lengo la kufanya biashara au kazi au chochote utakachoanza nacho ni kupata mtaji utakaokuwezesha kujiajiri au kufanya mambo yako mengine.
Usiogope kufanya au kujishughulisha na shughuli yeyote, hata ikiwa kujitwisha beseni la mboga mboga, na kutembeza wewe fanya ili mradi kichwani kwako uwe na target kwamba leo nafanya biashara hii kwa kutembeza, lengo langu ni nipate mtaji wa kufanya kitu flani, wakati nikiwa naendelea kutafuta  mtaji nitaboresha biashara yangu hii ili iendane na hadhi ninayoitaka, kama nilikua natembea kwa miguu, nitanunua baiskeli ili inirahisishie kazi na pia kuwafikia wateja wengi zaidi, kitakachofuata labda niwe na kituo changu cha usambazaji na niwe na watu wawili, watatu wa kunisaidia wakati huo nikiwa katika mchakato wa kuanzisha biashara yangu n.k


Lakini si vyema kuwahusisha watoto katika shughuli hizi na zinginezo za kibiashara na maendeleo kwa maana ya kujiajiri kwasababu utakuwa unamnyima mtoto fursa yake ya kuwa mtoto na kufanya mambo ya umri wake kama watoto wengine wa umri kama wake wanavyofanya ikiwa ni pamoja na elimu. Inawezekana kupiga hatua ya kimaendeleo, kujiajiri au hata kutimiza ndoto zako, anza leo tena anza na ulicho nacho. Hata katika imani zetu za  dini (kwa wanao amini uwepo wa Mungu kama mimi) Mungu alimruhusu Mussa (Moses) kufanya makubwa kwa kuanza na alicho nacho mkononi ambacho ni fimbo, kwahiyo hata wewe unaweza kufanya makubwa iwapo utatathubutu kuanza na ulichonacho.

"Magonjwa ya Akili ni magonjwa kama magonjwa mengine" Daktari Ruta(kitengo cha magonjwa ya akili hospitali ya taifa muhimbili)

Tarehe 08/02/2015 nilibahatika kuongozana na mdau na mwanaharakati mkubwa wa haki za wanawake na watoto, Joyce kiria kufuatilia tukio la mwanamke mmoja huko tabora ambae alifahamika kwa jina moja Bi Zuhura, kuwaua watoto wake wawili na kisha kuwafukia kwenye nyumba aliyokua anaishi. Safari yetu ilikua na changamoto nyingi ambapo gari ilituharibikia na hivyo tulilazimika kuchukua bus, ambayo ilitupa changamoto ya kusahau vifaa, kuchelewa n.k lakini tulifanikisha.
Kesho yake asubuhi tulianza safari ya kuelekea kwenye tukio, na kweli tulifika kwa msaada wa kapipi (mwandishi wa habari wa channel ten) ambaye alifuatilia kwa karibu tukio hili tangu siku ya kwanza lilivyotokea, na kwa habari tulizozipata hapo, kutoka kwa wahusika, yaani ndugu na majirani, pia mashuhuda wa tukio hilo kwa maana ya watu wa mwanzo walioona na pia kufuatilia tukio hilo ambae mmoja wapo, ni huyo mwandishi wa habari wa channel ten kuwa muhusika alikua na matatizo ya akili, na kwa maelezo yaliyotoka kwa babu yake Bi  Zuhura, mzee Shabani Ramadhani Kanene, faili la ugonjwa huo lilifunguliwa hospitali kitete Tabora na kwamba Bi Zuhura alipata ugonjwa huo mara baada ya kumzaa mtoto wake wa pili ambaye kwa sasa ni marehemu, ambapo inadaiwa aliuwawa na mama yake huyo baada  ya kumzidishia dawa alipokua anaumwa.
Mara baada ya kutoka eneo tukio hilo la kinyama lilipofanyika, safari ya kumtafuta baba mzazi wa marehemu ambae pia alikua mume halali wa Bi Zuhura, Bwana Mrisho ilianza, tulipata ushirikiano mzuri wa watu mbalimbali kutufikisha tulipopahitaji na muhusika (mume wa Bi Zuhura) alitueleza mambo mengi, likiwemo la kumuomba mana mzazi wa Bi Zuhura awachukue hao watoto kutokana na hali yake kiafya kutokua nzuri lakini Bi Zuhura na babu yake walikataa, alieleza.
Tuliporudi, tulimtafuta mtaalam wa magonjwa ya akili ambae ni daktari Ruta kutoka hospitali ya Taifa muhimbili, ambae alitueleza kuwa "magonjwa ya akili ni kama magonjwa mengine, na yanatibika iwapo yatawahi kupatiwa tiba ya uhakika, kwa kiwango kinachostahili na kwa wakati" alieleza zaidi kuwa wapo ambao wanapona kabisa na kurudi kwenye hali zao za kawaida, wapo ambao watatumia dawa maisha yao yote lakini wataweza kuendelea na shughuli zao za kila siku. Alisema magonjwa ya akili yapo ya aina makubwa na madogo,  na alisema tafsiri ya magonjwa ya akili ni magonjwa yanayoathiri mfumo mkubwa wa fahamu na kutibua visafirisha habari kwenye ubongo. 
Nilijifunza mengi na kwa hayo machache ni matumaini yangu na wewe umejifunza kitu, cha muhimu cha kuzingatia ni kwamba magonjwa ya akili yanaweza kumpata mtu yeyote, hivyo ni muhimu kuwafikisha katika vituo vya tiba watu wenaopatwa na matatizo hayo ili kuepusha madhara kwenye jamii yetu.

Monday, March 23, 2015

Harakati zangu kwenye mambo mbalimbali


Nilipata nafasi ya kuongozana na team nzima ya wanawakelive kwenda kufanya mahojiano na mshindi wa tuzo TWAA Jenifer Richard Shigoli, ambae alishinda  tuzo hiyo kupitia kipengele cha mwanamke mdogo mwenye mafanikio.
Hapa nilimuuliza baadhi ya maswali huyu shujaa wetu, kwa kweli nimejifumza mengi sana kupitia yeye. Alisema "Nilianza kutengeneza bidhaa zangu mwenyewe mara baada ya kumaliza Chuo kikuu Tumaini, ambapo bidhaa yangu ya kwanza niliitengeneza mwezi wa nane mwaka 2012. Nilianza kutengeneza bidhaa hizi za bulbby kwa mtaji wa shilingi elfu 23.
Hapa alinielezea kuhusu jinsi anavyofanya kufanikisha uuzaji wa bidhaa zake ambapo alisema baada ya kukabiliana na changamoto ya masoko na wateja aliamua kuja ma njia mbadala ya kukabiliana na changamoto hiyo ambayo ni kuanzisha kampeni ya Choo salama ambayo inajihusisha na kuisaidia jamii, mashuleni hasa shule za msingi katika kufanya usafi na pia kuwasambazia hizo bidhaa zake kwa nusu gharama. 

Saturday, March 14, 2015

Penye nia pana njia



Maisha ni vile  unavyoyataka yawe, ni vile unavyoyapigania na kuweka misimamo  thabiti na uwajibikaji. Chochote kile ambacho binadamu anaweza kukifikiria iwapo atakiamini na kukifanyia kazi kwa kujituma  bila kukata tamaa basi anaweza kukitimiza. Nilianza kuwa na ndoto za kufanya kazi kwenye runinga mwaka 2003 nikiwa darasa la nne. kwa wakati huo nilipenda kutangaza kipindi cha watoto ITV. Nilishiriki kwenye shindano la kutafuta mtangazaji wa kipindi cha watoto ITV lakini sikubahatika na licha ya hali hiyo sikukata tamaa niliamini siku moja nitatimiza lengo langu ilo.

Kwa kipindi hicho nilikuwa nikiimba na kuandika ngonjera, na mwaka 2004 nilirekodi nyimbo ambayo haikufanikiwa kuhit. Hata hivyo sikukata tamaa, nilishiriki kwenye mambo mbalimbali likiwemo Andika competition 2012 na kubahatika kuwa mshindni wa pili category politics(siasa) and economy(uchumi), n.k. Kuanzia 2011 nilikuwa nikitamani kumiliki kampuni yangu, na bado jitihada hizo zinaendelea. Lakini pia mwaka 2014 nilibahatika kupata nafasi ya kufanya kazi na Joyce Kiria (super woman) ambapo nafanya kazi mpaka ninapoandika hii post na nimeweza kujifunza vitu vingi na naendelea kujifunza kupitia yeye, hii yote ni kwasababu ya nia na malengo niliyonayo. Bado sijafika hata robo ya malengo yangu likiwemo la Kampuni, na hayo ni machache kati ya mengi ambayo nimewahi kuyafanya tangu kujitambua kwangu. Licha ya changamoto ninazokumbana nazo kila siku, bado napambana na huwenda mwaka huu nikatekeleza mipango yangu mingi zaidi. Penye nia, pana njia na nina imani malengo yangu yatatimia tu siku moja!!!