Tarehe 08/02/2015 nilibahatika kuongozana na mdau na mwanaharakati mkubwa wa haki za wanawake na watoto, Joyce kiria kufuatilia tukio la mwanamke mmoja huko tabora ambae alifahamika kwa jina moja Bi Zuhura, kuwaua watoto wake wawili na kisha kuwafukia kwenye nyumba aliyokua anaishi. Safari yetu ilikua na changamoto nyingi ambapo gari ilituharibikia na hivyo tulilazimika kuchukua bus, ambayo ilitupa changamoto ya kusahau vifaa, kuchelewa n.k lakini tulifanikisha.
Kesho yake asubuhi tulianza safari ya kuelekea kwenye tukio, na kweli tulifika kwa msaada wa kapipi (mwandishi wa habari wa channel ten) ambaye alifuatilia kwa karibu tukio hili tangu siku ya kwanza lilivyotokea, na kwa habari tulizozipata hapo, kutoka kwa wahusika, yaani ndugu na majirani, pia mashuhuda wa tukio hilo kwa maana ya watu wa mwanzo walioona na pia kufuatilia tukio hilo ambae mmoja wapo, ni huyo mwandishi wa habari wa channel ten kuwa muhusika alikua na matatizo ya akili, na kwa maelezo yaliyotoka kwa babu yake Bi Zuhura, mzee Shabani Ramadhani Kanene, faili la ugonjwa huo lilifunguliwa hospitali kitete Tabora na kwamba Bi Zuhura alipata ugonjwa huo mara baada ya kumzaa mtoto wake wa pili ambaye kwa sasa ni marehemu, ambapo inadaiwa aliuwawa na mama yake huyo baada ya kumzidishia dawa alipokua anaumwa.
Mara baada ya kutoka eneo tukio hilo la kinyama lilipofanyika, safari ya kumtafuta baba mzazi wa marehemu ambae pia alikua mume halali wa Bi Zuhura, Bwana Mrisho ilianza, tulipata ushirikiano mzuri wa watu mbalimbali kutufikisha tulipopahitaji na muhusika (mume wa Bi Zuhura) alitueleza mambo mengi, likiwemo la kumuomba mana mzazi wa Bi Zuhura awachukue hao watoto kutokana na hali yake kiafya kutokua nzuri lakini Bi Zuhura na babu yake walikataa, alieleza.
Tuliporudi, tulimtafuta mtaalam wa magonjwa ya akili ambae ni daktari Ruta kutoka hospitali ya Taifa muhimbili, ambae alitueleza kuwa "magonjwa ya akili ni kama magonjwa mengine, na yanatibika iwapo yatawahi kupatiwa tiba ya uhakika, kwa kiwango kinachostahili na kwa wakati" alieleza zaidi kuwa wapo ambao wanapona kabisa na kurudi kwenye hali zao za kawaida, wapo ambao watatumia dawa maisha yao yote lakini wataweza kuendelea na shughuli zao za kila siku. Alisema magonjwa ya akili yapo ya aina makubwa na madogo, na alisema tafsiri ya magonjwa ya akili ni magonjwa yanayoathiri mfumo mkubwa wa fahamu na kutibua visafirisha habari kwenye ubongo.
Nilijifunza mengi na kwa hayo machache ni matumaini yangu na wewe umejifunza kitu, cha muhimu cha kuzingatia ni kwamba magonjwa ya akili yanaweza kumpata mtu yeyote, hivyo ni muhimu kuwafikisha katika vituo vya tiba watu wenaopatwa na matatizo hayo ili kuepusha madhara kwenye jamii yetu.
No comments:
Post a Comment